SGBV1

Ghasia Mwaka wa 2007-08: Waathiriwa Bado Wasubiri Haki

Ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-08 nchini Kenya zilisababisha maafa mengi, wanawake na na watoto wa kike kunajisiwa na kubakwa, mali kuporwa na wakenya kuwa wakimbizi katika nchi yao. Katika hali hiyo ya vita, ilikuwa vigumu sana kuripoti visa hivyo kwa polisi na hata kupata matibabu ya dharura. Kuna wahusika wachache sana ambao walishtakiwa mahakamani lakini kesi zikatupiliwa mbali kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Kikundi cha waathiriwa ambao walinajisiwa kiliwasilisha kesi mahakamani, kesi nambari 122 ya mwaka 2013 katika Mahakama Kuu ya Kenya. Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yakiwemo, the Kenyan Section of the International Commission of Jurists, Coalition on Violence Against Women, Physicians for Human Rights na Independent Medico Legal Unit viliwasaidia waathiriwa hao kuwasilisha kesi mahakamani dhidi ya Mwanasheria Mkuu na maafisa wengine wa serikali.

Kuna mambo kadha wa kadha ambayo mahakama inafaa kufanyanyia maamuzi yakiwemo jambo la ridhaa kwa waathiriwa wa kesi za ubakaji. Kenya ilikua na jukumu kuu la kuwalinda wakenya na kufanya uchunguzi kuhusiana na vita vilivyotokea baada ya uchaguzi. Hata hivyo serikali ya Kenya ilishindwa kufanya hivyo. Kwa sasa waathiriwa hao wanaiomba mahakama iamuru serikali ya Kenya kuwapa ridhaa na matibabu kwa wanawake ambao walinajisiwa. Pia kuna zile rekodi ambazo ni muhimu katika kesi hiyo zinazohitajika kutolewa ili zitumike mahakamani au zi ifadhiwe vyema.

Katika mseto wa sheria za Kenya zinazowalinda waathiriwa ambao wamenajisiwa au kubakwa,ni muhimu kuongelea mambo fulani. Ni dhahiri ya kwamba vita vilitokea mwaka 2007-08 na wakenya waliathirika. Jambo la kwanza kuangaziwa ni jinsi serikali ya Kenya ilikuwa imejizatiti kuwalinda wakenya. Polisi ambao walikua wametumwa kuwalinda wakenya hawangetosha. Mbali na hayo, polisi wengine walijihusisha na visa vya unajisi na ubakaji. Kuna baadhi ya waathiriwa ambao walijaribu kuripoti kesi hizo japo hawangeweza.Labda kwa sababu ya uoga au aibu ambayo inaambatana na kesi za kunajisiwa au kubakwa. Baadhi ya waathiriwa walinyimwa fursa ya kurekodi kesi zao kwa polisi.

Sheria za Kenya zimeandikwa kwa ufasaha. Katiba ya Kenya inazungumzia kuhusu haki za mkenya. Katiba pia inakubali sheria za kimataifa kutumika humu nchini. Idara ya mahakama ya Kenya iko na jukumu la kusoma sheria hizi na kuamua kesi kulingana na ushahidi ambao umetolewa mahakamani. Waathiriwa wa visa vya ubakaji na unajisi ni kitengo ambacho kinahitaji kushughulikiwa kwa umakini sana. Wengi wa Waathiriwa hao huwa na shida za kisaikolojia kwa sababu ya vitendo ambavyo walifanyiwa. Waathiriwa hao pia huhofia maisha yao haswa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007. Hii ni kwa sababu bado wanaishi na wabakaji hao na kesi hizi mara kwa mara hulinganishwa na kesi ambayo iliwasilishwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai(ICC). Bila ulinzi wa kutosha kutoka kwa serikali, waathiriwa hao hawawezi kutoa ushahidi mahakamani kwa amani.

Kwa kawaida, kesi zilizo na uzito kama za ubakaji na unajisi huchukua muda mrefu kumalizika mahakamani. Waathiriwa hao wanahitaji usaidizi hata kesi zinapoendelea. Kuna waathiriwa ambao waliambukizwa virusi vya HIV vinavyosababisha UKIMWI na maradhi mengine ya zinaa. Wengine waliathirika kisaikolojia na wanahitaji matibabu na ushauri. Kesi inapokawia mahakamani, waathiriwa wanaendelea kuishi katika hali hiyo. Kesi hii ilichukua muda mrefu kabla ya kuanza mahakamani. Serikali ya Kenya haikuwa tayari kujiwasilisha mahakamani ili kesi isikilizwe na kumalizwa kwa muda muafaka.

Iwapo kesi hii itamalizika mahakamani na maombi ya waathiriwa kutimizwa, basi haki itakuwa imetendeka. Kesi hii itaonyesha ya kwamba serikali ya Kenya haiwezi kukwepa jukumu lake la kuwalinda wananchi. Jukumu la kufanya uchunguzi na kuwashtaki wahusika ni la serikali. Iwapo wanalemewa au kuzembea katika kulitekeleza jukumu hilo, mahakama inafaa kuingilia kati na kuhakikisha waathiriwa wanapata haki.

Leave a Reply
Previous Article

Tenders

Next Article

Tender

Related Posts